Social Icons

Sikiliza Tone Radio Live Hapa, na Tembelea Website yetu www.toneradiotz.com

bre

Thursday, May 9, 2013

ZAHANATI YAGEUZWA OFISI YA AFISA MTENDAJI MBARALI MBEYA

JENGO LA LA OFISI YA AFISA MTENDAJI LILILOBOMOKA SASA WAMEHAMIA KATIKA ZAHANATI




HII NDIYO ZAHANATI ILIYOVAMIWA NA MTENDAJI NA KUFANYWA OFISI YA MTENDAJI 


JENGO LA ZAHANATI HIYO SASA NI OFISI YA MTENDAJI 






KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida, Uongozi wa Serikali ya Kijiji cha Mpolo kata ya Utengule Wilaya ya Mbarali Mkoa wa Mbeya imegeuza matumizi ya Zahanati ya Kijiji kuwa Ofisi.
             
Hilo limebainika baada ya Waandishi wa Habari kutembelea eneo hilo na kukuta majengo ya Zahanati hiyo yakitumika kama Ofisa ya Mtendaji wa Kijiji, Ofisi ya Mwenyekiti na Ofisi kwa ajili ya Baraza la Usuluhishi la Kijiji.

Mwenyekiti wa Kijiji hicho Andres Mlongosi,  alipohojiwa kuhusiana na tuhuma za kugeuza matumizi ya Jengo ambalo lilitakiwa litumike kwa ajili ya Zahanati lakini wao wanalitumia kama ofisi alikiri kufanya kinyume kwa kile alichodai Serikali ya Kijiji haina ofisi kutokana na jengo lilikuwa likitumika awali kubomoka.

Aliongeza kuwa wako kwenye mpango wa kujenga upya ofisi yao ambapo baada ya kukamilika Jengo hilo litaachwa litumike kama ilivyokuwa imekusudiwa kwa matumizi ya Zahanati ambapo hadi sasa Wananchi hupata matibabu katika Kituo cha Afya cha Utengule, Igurusi au Hospitali ya Misheni ya Chimala sehemu ambazo ni mbali.

Aidha wananchi hao wameendelea kupata adha ya matibabu hasa Wanawake wajawazito ambao hutumia muda mrefu kusafiri kufuata matibabu pamoja na Wazee wasiojiweza ambapo hutembea kwa zaidi ya Kilomita 15.

Kwa upande wake Afisa Mtendaji wa Kata ya Utengule, Benyanga Zuberi amethibitisha uwepo wa hali hiyo na kwamba Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali  ndiyo iliyosababisha hali hiyo kutokana na kutotuma fedha za kumalizia maeneo yaliyobaki kama Choo.

Alisema suala la kuweka Ofisi kwenye majengo ya Zahanati ni suala la Mpito ambapo baada ya kukamilika kwa ujenzi kwa asilimia zote Zahanati itaendelea kama kawaida hivyo Wananchi wasiwe na wasiwasi kuhusu hali hiyo.

Nao Wananchi wa Kijiji hicho walisema wanasikitishwa na kitendo kilichofanywa na uongozi wa Kijiji cha kugeuza majengo ya Zahanati kuwa ofisi licha ya kutumia nguvu nyingi kuchangia ujenzi huo.

Walisema kitendo hicho si cha uungwana na kinakatisha tamaa wananchi kuendelea kujitolea nguvu na michango katika kufanikisha ujenzi na shughuli mbalimbali za maendeleo kama wataendelea kugeuza matumizi tofauti na inavyokuwa imekusudiwa.

Diwani wa kata ya Utengule Juntwa Mwalyaje alikiri kuwepo kwa tatizo hilo na kwamba Baraza la dharula lililoketi Mei 6, Mwaka huu lilikutana kujadili mustakabali wa zahanati hiyo ambapo walimwomba mganga Mkuu wa Wilaya kuandika barua ya maombi ya fedha za kumalizia ujenzi wa zahanati hiyo ikiwemu ujenzi wa Choo na Nyumba ya Mganga.

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Wilaya ya Mbarali Venance Gwaza Mwashala amesema Halamashauri ilishapitisha Shilingi Milioni Tano kwa ajili ya ujenzi wa awamu ya Kwanza ambazo zitaingizwa katika akaunti ya Kijiji wakati wowote kuanzia sasa

Aidha ameutaka uongozi wa kijiji kuongeza nguvu zao ili waweze kukamilisha mapema ujenzi huo na kuletewa waganga na huduma zote ili kupunguza adha kwa wananchi ya kufuata matibabu mbali.

Picha na E.Kamanga 

No comments: