Social Icons

Sikiliza Tone Radio Live Hapa, na Tembelea Website yetu www.toneradiotz.com

bre

Tuesday, June 4, 2013

TAARIFA YA CHAMA CHA WAANDISHI WA HABARI MKOA WA MBEYA KWA VYOMBO VYA HABARI TAREHE 04. 06. 2013.

MWANDISHI WA HABARI RASHID MKWINDA ALIEPATA MADHARA


MBEYA PRESS CLUB
TAMKO LA CHAMA CHA WAANDISHI WA HABARI MKOA WA MBEYA LA KULAANI KUPIGWA KWA MWANDISHI WA HABARI RASHID MKWINDA WAKATI WA MECHI YA MPIRA WA MIGUU BAINA YA KIMONDO FC NA NJOMBE FC ILIYOFANYIKA JUNI 2 KATIKA UWANJA WA KUMBUKUMBU YA SOKOINE JIJINI MBEYA.

JUNI 2, mwaka huu kulikuwa na mechi ya mpira wa miguu ya Ligi ya Mabingwa wa mikoa baina ya timu ya Kimondo FC ya Mbozi mkoani Mbeya na Njombe FC ya Mkoa mpya wa Njombe, mchezo uliofanyika katika uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine Jijini Mbeya.

Wakati mchezo huo ukiendelea, wandishi wa habari kama ilivyo kawaida yao walifika uwanjani hapo kutekeleza wajibu wao wa kuchukua habari na kuuhabarisha umma wa watanzania.
Wakati wa mapumziko ulipofika, wachezaji wa Timu ya Kimondo FC waliingia kwenye chumba chao cha kubadilishia nguo, lakini wachezaji wa timu ya Njombe FC hawakwenda kwenye chumba chao cha kubadilishia nguo na badala yake walibakia uwanjani na kwenda kukaa mahali lilipokuwa benchi la ufundi la timu hiyo.

Mwandishi wa Habari wa Gazeti la Majira Rashid Mkwinda ambaye pia ni mwanachama wa Chama cha Wandishi wa Habari Mkoa wa Mbeya alikwenda kuwapiga picha wachezaji hao ambao kwa wakati huo walikuwa pamoja na viongozi wa timu hiyo.
Kitendo hicho kilisababisha golikipa wa timu ya Njombe FC, Joshua Mwampegeje kuanza kumtolea matusi mwandishi huyo, huku wachezaji wengine pamoja na viongozi wao wakimfuata na kuanza kumpiga, kumjeruhi, kusababishia uvimbe na maumivu mwilini na kumvunjia kamera yake wakati akitimiza wajibu wake.

Mashabiki wa Njombe FC waliokuwa Jukwaani walipoona vurugu hizo nao waliingia uwanjani na kushirikiana na viongozi na wachezaji wa timu yao kumpiga mwandishi na kumjeruhi.
Tukio hilo lilikuwa likishuhudiwa na viongozi wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Mbeya (MREFA) ambao walikuwa wamekaa kwenye jukwaa kuu wakishuhudia kila kitu kilichokuwa kikiendelea uwanjani hapo bila ya kuchukua hatua yoyote.

Aidha wachezaji hao walifanikiwa kumpiga, kumjeruhi na kumvunjia kamera mwandishi huyo kutokana na kutokuwepo kwa ulinzi wa aina yoyote uwanjani hapo, hali ambayo pia ilisababisha mashabiki kuingia kirahisi uwanjani na kuongeza ukubwa wa vurugu.
Kutokana na kitendo hicho, Chama cha Wandishi wa Habari Mkoa wa Mbeya kinalaani vikali kitendo cha mwandishi Rashid Mkwinda kupigwa, kujeruhiwa na kuharibiwa zana zake za kazi wakati akitimiza wajibu wake, kikiamini kuwa kitendo hicho hakikuwa cha kistaarabu hata kidogo, kwani ni ukiukwaji mkubwa haki za binadamu na uvunjaji wa Uhuru wa vyombo vya habari nchini.

Hivyo basi, Chama cha Wandishi wa Habari Mkoa wa Mbeya kinakitaka Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Mbeya kutoa tamko kuhusiana na tukio hilo, kikielezea hatua zilizochukuliwa kuiadhibu timu ya Njombe FC kwa kitendo cha kumpiga mwandishi wa habari.


Chama cha Wandishi wa Habari Mkoa wa Mbeya pia kinalitaka Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kuchukua hatua kwa mujibu wa kanuni na sheria za soka nchini dhidi ya wahusika ili kuhakikisha matukio ya aina hiyo hayajirudii mahali popote nchini.

Chama cha Wandishi wa Habari Mkoa wa Mbeya kinajiuliza sababu za mchezo huo kufanyika bila ya kuwepo kwa ulinzi wa aina yoyote uwanjani hapo, kwani tunaamini kuwa mchezo huo ulistahili kupewa ulinzi wa Polisi kwa mujibu wa sheria za nchi, kwa sababu huwenda uwepo wa ulinzi uwanjani hapo ungepunguza ukubwa na athari za vurugu hizo.





Nakala kwa:
1.       Umoja wa Club Tanzania (UTPC)
2.       Baraza la Habari Tanzania (MCT)
3.       Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
4.       Chama Cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Mbeya (MREFA)
5.       Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya
6.       Njombe FC
7.       Kimondo FC
8.       Vilabu vya Wandishi wa Habari vya Mikoa yote Tanzania
9.       Vyombo vya Habari




1 comment:

Anonymous said...

Ipo haja kwa waandishi wenyewe kuchukua tahadhari wakati fulani wanapofanya shughuli zao, mfano kusoma hali ya mchezo ilivyo, tabia za mashabiki, usalama uliopo uwanjani, eneo la kujihami endapo lolote litatokea,pia kabla yatamko uongozi wa mbeya press club ungekutana na MREFA kwa kuwa wanakitengo cha habari