Social Icons

Sikiliza Tone Radio Live Hapa, na Tembelea Website yetu www.toneradiotz.com

bre

Sunday, September 8, 2013

HONGERA MICHUZI BLOG KWA KUTIMIZA MIAKA TISA

SALAM MAALUM KUTOKA KWA LIBENEKE LA MICHUZI

 Ankal akipongezwa na blogger gwiji duniani kaka Ndesanjo Machas iku alipoanzisha rasmi Globu ya Jamii katika ukumbi wa mikutano wa Finlandia jijini Helsinki, Finland, Septemba 8, 2005
 Ankal na mai waifu wake na toto tundu Sellah wakikata keki kuadhimisha miaka 9 ya Globu ya Jamii usiku wa kuamkia leo
-----------------------------------------------------------
Ilikuwa siku ya Alhamisi tarehe kama ya leo (Septemba 8,) miaka TISA iliyopita wakati Globu ya Jamii ilipozaliwa rasmi katika ukumbi wa mikutano wa Finlandia jijini Helsinki Finland, kama utani tu. Kwa msemo mwingine, ni miaka TISA kamili leo toka Globu ya Jamii ianze Libeneke la kuhabarisha wadau kwa mapicha na habari kemkem bila kukosa hata siku moja
Kikosi kazi cha Globu ya Jamii kingependa kutoa shukrani za dhati kwa wadau wote duniani kote kwa kampani mnayotupa kila saa, siku, wiki, miezi na hadi sasa ikiwa ni MIAKA TISA kamili.  Si jambo dogo, ukizingatia katika safari hii njiani tumekutana na kila aina ya changamoto, kubwa kuliko yote ikiwa ni kufanya kila tuwezalo kubakia hapa tulipo kwa kufuata weledi pamoja na sera ya HATUBAGUI, HATUCHAGUI; ATAYETUZIKA HATUMJUI, pamoja na kauli mbiu kwa wadau watoa maoni ya kuwa waangalifu kutochafua hali ya hewa wala kujeruhi hisia ya mtu wakati wa kutoa maoni.
Si rahisi kumridhisha kila mdau, na kwa mujibu wa usemi wa Kimombo wa “What’s good for the goose is bad for the hen” unaomaanisha hivyo. Yaani “Kilicho kizuri kwa bata mzinga, ni kibaya kwa kuku”.
Katika kuadhimisha hii MIAKA TISA ya Libeneke, Globu ya Jamii haitofanya sherehe ya pamoja na wadau kama ilivyotarajiwa. Badala yake Ankal kajikakamua na kununua kajikeki na kukata na kula na familia kwa niaba ya wadau. Ila ahadi yetu ni kwamba, panapo majaaliwa, sherehe kubwa itaandaliwa mwakani wakati wa kuadhimisha MIAKA KUMI. Ni mapema mno kusema itakuwaje, ila panapo uhai itakuwa  SHEREHE KUBWA na inayostahili.
Kwanza kabisa tunamshukuru Jalali Muumba wa vyote kwa tunu hii aliyoitupa. Tunatambua kuwa tuna bahati ya sisi kuwa sisi, na kamwe bahati hiyo uliyotupa, EWE MOLA, hatutoichezea...
Globu ya Jamii pia inachukua nafasi hii kuwashukuru wadhamini wake, ikiwa ni pamoja na VODACOM, AIRTEL, UHURU ONE,  TTCL, NMB, NBC, AZANIA BANK, CRDB, NHC, PRECISION AIR, AIR UGANDA, NSSF, PSPF, DSTV, SKYLINK, SERENGETI FREIGHT FORWADERS  ‘WAZEE WA KAZI’, SWIFT FREIGHT, GIRAFFE OCEAN VIW HOTEL, DR MKOMBOZI,  na wengineo wote. Tunashukuru kwa kutuamini na kuendelea kuendeleza nasi Libeneke. 
Shukrani zingine  za kipekee ziende kwa familia yangu kwa uvumilivu wanaoonesha kwangu, pia kwa wadau kadhaa ambao tukiamua kuwataja wote hapa itachukua ukurasa wote hu na tusiwe tumetaja japo robo yao. Kwa uchache tu, na ambao ni kwa niaba ya wale ambao hatutotaja kwa ufinyu wa nafasi na pia si  kwa ubora wao, shukrani hizo zimwendee kaka Ndesanjo Macha kwa kuwa wa kwanza kutufungulia na kutuongoza njia na kutupa maudhui ambao baada ya kuyafuata, tumeona faida yake.
Washauri wakuu wetu pia hatuwasahau katika hili. Nao  ni Profesa Mark Mwandosya, Mhe. January Makamba, Freddy Macha, Balozi Peter Kallaghe, Othman Michuzi, Ahmad Michuzi, Christopher Makwaia MK, Steve Wassira jnr., Nathan Chiume, DJ Luke Joe wa Vijimambo, Waziri Ally, John Kitime, Alex Perullo, Muhidin Maalim Gurumo, kaka Jeff Msangi, Boniface Makene, Kirk Gills, Oscar Shelukindo, Ephraim Mafuru, Imani Kajula, Profesa Mbele, Da' Chemi Chemponda, Ankal Beda Msimbe, kaka Assah Mwambene, Da' Tagie Daisy Mwakawago, Shamim Zeze wa 8020 Fashions, Mama wa Mitindo Asia Idarous na mumewe Mzee Khamsin, Ainde, kaka Asimwe Kabuga, Abdallah Ezza na Fide Tungaraza wa Heslsinki na wengineo wengi tu. Ushauri wenu tunauthamini na kuuheshimu!
Wengine ni viongozi wote wakuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,  Spika, Naibu Spika na maofisa wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Waheshimiwa Wabunge wote wa Jamhuri ya Muungano pamoja na wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Viongozi  maofisa wote wa vyama vya siasa, Viongozi wote na watumishi  wa taasisi za umma na binafsi, Mablogger wote na mwisho ni wadau wote wanaotupa moyo kila kukicha. Asanteni sana, sana,  sana, sana. Hatuna cha kuwapa zaidi ya hizo SHUKURANI kutoka katika kilindi cha moyo wetu. MOLA AWE NANYI, NA AWAZIDISHIE PALE PALIPOPUNGUA.
Hatuna la zaidi la kusema zaidi ya kuahidi kwamba tutaendeleza Libeneke kwa moyo wetu wote huku tukipiga magoti kuwaomba wapendwa wadau wetu duniani kote muendelee kutupa kampani, kwani bila ninyi sisi si lolote si chochote. Pia tunaomba radhi pale tunapoteleza kama binaadamu yeyote ambaye daima duni si mkamilifu, ambapo likitokea litalotokea si kwa makusudi ama nia mbaya bali ni kwa udhaifu huo huo wa kibinaadamu.

Naomba kuwasilisha,
Wenu Mnyenyekevu,
Muhidin Issa Michuzi “Ankal”


TONE MULTIMEDIA GROUP TUNATOA PONGEZI ZETU ZA DHATI KWA GLOBU  YA JAMII KWA KUFIKISHA MIAKA TISA TANGU IANZE KAZI ZAKE. TUNAWATAKIA MAFANIKIO MEMA. HONGERA SANA MUHIDIN ISSA MICHUZI NA TIMU YAKO NZIMA





No comments: